Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Mei 04, 2024 Local time: 15:05

Uganda yaweka mikakati ya kukuza miji mikubwa


Jiji la Kampala, Uganda. Picha na AFP
Jiji la Kampala, Uganda. Picha na AFP

Wabunge wanane wa Uganda wako Nairobi Kenya kwa ziara ya mafunzo juu ya  kushughulikia changamoto za ukuaji wa miji nchini humo ikiwemo udhibiti makazi duni na kupitisha sera mahiri za ukuaji wa miji mikubwa.

Wabunge hao wa Kamati ya Jinsia, Leba na Maendeleo ya Jamii ya Bunge la Uganda watajaidili juu ya makazi ya jamii za watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda inayohausishwa katika mpango wa kitaifa wa kujenga nyumba za kisasa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge la Uganda ya Jinsia, Leba na Maendeleo ya Jamii, Rwabushaija Margaret Namubiru amevieleza vyombo vya habari kuwa mafunzo ya ziara hii yanahusu hatua muhimu za kuchukuliwa ili kuendeleza miji ya kisasa nchini humo.

Amesema kuwa Kamati hiyo itaongoza serikali ya Uganda kuhusu jinsi inavyoweza kushirikiana na sekta ya kibinafsi na mashirika ya kiraia ili kuunga juhudi za kufanikisha ujenzi na ukuaji wa miji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya makazi bora na salama kwa raia wa Uganda.

Charles Bakkabulindi, mbunge wa Uganda katika ziara hiyo, ameeleza kuwa iwapo Afrika inataka kufanikiwa katika ujenzi wa miji ya kisasa, ni sharti vijana wawe sehemu ya juhudi hizo za kitaifa.

Uganda inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile makazi duni, uhaba wa huduma muhimu, ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana, uwezo dhaifu wa usimamizi wa miji na upungufu mkubwa wa fedha. Zaidi ya hayo hivi sasa inakabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, na uhaba wa miundombinu.

Eneo la makazi duni la Banda huko Uganda
Eneo la makazi duni la Banda huko Uganda

Serikali ya nchi hiyo inakadiria hadi kufikia mwaka 2035 idadi ya watu nchini Uganda itafikia milioni 68.4 ambapo 30% yao itakuwa wakiishi mijini, na matatizo hayo yanaweza kuongezeka iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Nchini Kenya, zaidi ya asilimia 60 ya raia wake wanaoishi mijini wako katika vitongoji duni, na baadhi wao wanaishi katika nyumba zisizo nzuri.

Kenya imeteua idara ya huduma za nyumba na makazi kama nguzo ya nne kati ya tano za utekelezaji wa agenda ya serikali ya rais William Ruto ya miaka mitano wakati kuna mahitaji ya makazi mapya mijini yanayokadiriwa kuwa nyumba 250,000 kwa mwaka.

Kufanikisha ajenda hiyo, Ruto ameapa kutekeleza mpango wa nyumba za bei nafuu utakaolenga makundi ya makazi ya kijamii ya wenye kipato cha chini ya shilingi 20,000, nyumba za bei nafuu zinazo kenga watu wenye kipato cha kati ya shilingi elfu 21,000 na elfu 149,000 pamoja na makazi ya soko nafuu linalowalenga watu wenye mapato ya kila mwezi ya zaidi ya shilingi elfu 150,000.

Mpango wake ni kujenga nyumba zaidi ya 200,000 kwa watu wa kipato cha chini kila mwaka nchini Kenya ni njia ya kuwezesha kupatikana kwa takriban nafasi za kazi milioni mbili katika uchumi wa Kenya.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera Sauti ya Amerika, Nairobi.

Forum

XS
SM
MD
LG